'Wahamiaji wote wanapaswa kumlipa msafirishaji haramu... lakini wanawake wanalazimika kutoa huduma za ngono'

Mwanamke akiwa amesimama ameelekeza macho kwenye kamera
Maelezo ya picha, Esther alikimbia Lagos mwaka wa 2016
    • Author, Sofia Bettiza
    • Nafasi, Global Health Reporter
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Esther alikuwa amelala mitaani jijini Lagos wakati mwanamke mmoja alipomkaribia na ahadi ya njia ya kutoka Nigeria kwenda kazini na nyumbani barani Ulaya.

Alikuwa ameota maisha mapya, hasa Uingereza. Akiwa amefukuzwa kutoka katika nyumba ya malezi yenye vurugu na yenye lugha chafu, hakuwa na sababu ya kukaa.

Lakini alipoondoka Lagos mwaka wa 2016, akivuka jangwa hadi Libya, hakuwa na wazo lolote kuhusu safari yake ya kutisha iliyo mbele yake, kulazimishwa kufanya kazi ya ngono na miaka mingi ya madai ya hifadhi katika baada ya nchi.

Wahamiaji wengi wasio wa kawaida na wanaotafuta hifadhi ni wanaume, 70% kulingana na Shirika la Ulaya la Hifadhi, lakini idadi ya wanawake kama Esther, ambao wamekuja Ulaya kutafuta hifadhi inaongezeka.

"Tunaona ongezeko la wanawake wanaosafiri peke yao, katika njia za Mediterania na Balkan," anasema Irini Contogiannis kutoka Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji nchini Italia.

Ripoti yake ya 2024 ilionesha ongezeko la kila mwaka la 250% la idadi ya wanawake wazima wasio na waume wanaofika Italia kwa njia ya Balkan, huku familia zikiongezeka kwa 52%.

Njia za wahamiaji zinajulikana kuwa hatarini. Mwaka jana vifo 3,419 vya wahamiaji au kutoweka barani Ulaya vilirekodiwa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), mwaka mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa.

Lakini kwa wanawake, kuna tishio la ziada la unyanyasaji wa kijinsia na unyonyaji, ambalo lilimtokea Esther baada ya kusalitiwa na mwanamke ambaye alikuwa amemuahidi maisha bora.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Alinifungia chumbani na kumleta mwanaume. Alifanya ngono nami, kwa nguvu. Nilikuwa bado bikira," Esther anasema. "Hicho ndicho wanachofanya ... husafiri hadi vijiji tofauti nchini Nigeria kuchukua wasichana wadogo, na kuwaleta Libya kuwa watumwa wa ngono."

"Uzoefu wao ni tofauti na mara nyingi ni hatari zaidi," Ugochi Daniels wa IOM aliiambia BBC. "Hata wanawake wanaosafiri katika vikundi mara nyingi hukosa ulinzi thabiti, na kuwaweka katika hatari ya kutendewa vibaya na wasafirishaji haramu, wafanyabiashara haramu, au wahamiaji wengine."

Wanawake wengi wanajua hatari hizo lakini huenda hata hivyo, kufungasha kondomu, au hata kuweka vifaa vya uzazi wa mpango iwapo watabakwa njiani.

"Wahamiaji wote wanapaswa kumlipa msafirishaji haramu," anasema Hermine Gbedo wa mtandao wa kupambana na biashara haramu ya binadamu Stella Polare. "Lakini wanawake mara nyingi wanatarajiwa kutoa ngono kama sehemu ya malipo."

Bi. Gbedo anawaunga mkono wanawake wahamiaji huko Trieste, jiji la bandari kaskazini-mashariki mwa Italia ambalo kwa muda mrefu limekuwa njia panda ya tamaduni na hutumika kama kiingilio kikubwa cha Umoja wa Ulaya kwa wale wanaovuka kutoka Balkan. Kuanzia hapa, wanaendelea hadi nchi kama Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza.

 v

Chanzo cha picha, Barbara Zanon/Getty Image

Maelezo ya picha,

Baada ya miezi minne ya kunyonywa nchini Libya, Esther alitoroka na kuvuka Bahari ya Mediterania akiwa kwenye boti la mpira ambalo aliokolewa na walinzi wa pwani wa Italia na kupelekwa kisiwa cha Lampedusa.

Alidai hifadhi mara tatu kabla ya kupewa hadhi ya ukimbizi.

Watafuta hifadhi kutoka nchi zinazoonekana kuwa salama mara nyingi hukataliwa.

Wakati huo Italia iliiona Nigeria kama isiyo salama, lakini miaka miwili iliyopita ilibadilisha tathmini hiyo huku serikali kote Ulaya zikianza kuimarisha sheria zao ili kukabiliana na wimbi kubwa la wahamiaji kuingia Ulaya mwaka 2015-16.

Sauti zinazotaka vikwazo zaidi kuhusu madai ya hifadhi zimeongezeka tu tangu wakati huo.

"Haiwezekani kuendeleza uhamiaji wa watu wengi, hakuna njia," anasema Nicola Procaccini, mbunge katika serikali ya mrengo wa kulia ya Giorgia Meloni. "Tunaweza kuwahakikishia maisha salama wanawake hao ambao wako hatarini, lakini si wote."

"Lazima tuwe wagumu," anaonya Rakib Ehsan, Mwanachama Mkuu katika shirika la la Think tank Policy Exchange,. "Tunahitaji kuwapa kipaumbele wanawake na wasichana walio katika hatari ndani ya maeneo yaliyoathiriwa na migogoro, ambapo ubakaji unatumika kama silaha ya vita."

Kwa sasa hili halifanyiki mara kwa mara, anasema, na ingawa anasikitikia hali ya wanawake wanaokabiliwa na njia hatarishi za kuingia Ulaya.

Hata hivyo, wanawake wengi wanaofika kutoka nchi zinazochukuliwa kuwa salama wanadai kwamba unyanyasaji waliopata kwa sababu ya kuwa wanawake umemaanisha kuwa maisha katika nchi zao yamekuwa magumu.

Hii ilikuwa kesi kwa Nina, mwenye umri wa miaka 28 kutoka Kosovo.

"Watu wanafikiri kila kitu kiko sawa Kosovo, lakini hiyo si kweli," anasema. "Mambo ni mabaya kwa wanawake."

Nina anasema yeye na dada yake walinyanyaswa kingono na wapenzi wao wa kiume ambao waliwalazimisha kufanya kazi ya ngono.

Ripoti ya 2019 ya shirika la usalama la OSCE la Ulaya ilisema kwamba 54% ya wanawake huko Kosovo wamepitia unyanyasaji wa kisaikolojia, kimwili au kingono kutoka kwa wenzi wa karibu tangu umri wa miaka 15.

Wanawake wanaokabiliwa na mateso kwa misingi ya ukatili wa kijinsia wana haki ya kupata hifadhi chini ya Mkataba wa Istanbul wa Baraza la Ulaya, na hilo liliungwa mkono na uamuzi muhimu wa mahakama kuu ya EU mwaka jana.

Mkataba huo unaelezea ukatili wa kijinsia kama wa kisaikolojia, kimwili na kingono, na unajumuisha ukeketaji wa wanawake (FGM).

Hata hivyo, masharti yake bado hayatumiki mara kwa mara, kulingana na vikundi vya hisani.

"Maafisa wengi wa hifadhi katika uwanja huu ni wanaume ambao hawajafunzwa vya kutosha kushughulikia suala nyeti kama hilo [kama ukeketaji wa wanawake], kiafya na kisaikolojia," anasema Marianne Nguena Kana, Mkurugenzi wa Mtandao wa Ulaya wa End FGM.

Maombi ya hifadhi ya wanawake wengi yamekataliwa, anasema, kwa dhana potofu kwamba, kwa sababu tayari wamefanyiwa ukeketaji, hawakabiliwi na hatari zaidi.

"Tumekuwa na majaji wakisema: 'Tayari umekeketwa, kwa hivyo si hatari kwako kurudi nchini kwako, kwa sababu si kama wanaweza kukufanyia tena," Nguena Kana anasema.

wanawake

Chanzo cha picha, International Rescue Committee

Maelezo ya picha,

Linapokuja suala la ukatili wa kijinsia, Carenza Arnold kutoka shirika la hisani la Uingereza la Women for Refugee Women anasema mara nyingi ni vigumu kuthibitisha, kwani haliachi makovu sawa na mateso ya kimwili na miiko na tamaduni kwa wanawake hufanya mchakato huo kuwa mgumu zaidi.

"Mara nyingi wanawake huharakishwa kupitia mchakato huo na huenda wasifichue ukatili wa kijinsia walioupata kwa afisa wa uhamiaji ambaye wamekutana naye hivi karibuni," Arnold anaelezea.

Ukatili mwingi unaowakabili wanawake hufanyika wakati wa safari yao, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limeiambia BBC.

"Kwa kawaida wanawake hutoroka ukatili wa kijinsia kutoka kwa wenzi wao katika nchi yao ya asili, na kisha wakati wa safari, hupata uzoefu huo tena," anasema Ugochi Daniles.

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Nina na dada yake katika safari yao ya kuwaacha wenzi wao wanyanyasaji huko Kosovo kuelekea maisha mapya nchini Italia.

Wakisafiri na wanawake wengine, walitembea kupitia misitu ya Ulaya Mashariki wakijaribu kuepuka mamlaka. Huko, walisema walishambuliwa na wahamiaji wanaume na wasafirishaji haramu.

"Ingawa tulikuwa juu milimani, gizani, ungeweza kusikia mayowe," Nina anakumbuka. "Wanaume hao walitujia wakiwa na tochi, waliziwasha nyusoni mwetu, kuchagua wanaomtaka, na kuwapeleka zaidi msituni.

"Usiku, niliweza kumsikia dada yangu akilia, akiomba msaada."

Nina na dada yake waliwaambia mamlaka ya Italia kwamba wakirudi nyumbani wangeuawa na wapenzi wao wa zamani. Hatimaye walipewa hifadhi.

Mapambano ya Esther ya hadhi ya ukimbizi yalichukua muda mrefu zaidi.

Alidai hifadhi kwa mara ya kwanza nchini Italia mwaka wa 2016, lakini baada ya kusubiri kwa muda mrefu huko alihamia Ufaransa na kisha Ujerumani, ambapo madai yake ya hifadhi yalikataliwa kwani kulingana na kanuni ya EU ya Dublin, mwombaji hifadhi kwa kawaida anatarajiwa kuomba hifadhi katika nchi ya kwanza ya EU anayoingia.

Hatimaye alipewa hadhi ya ukimbizi nchini Italia mwaka wa 2019.

Karibu muongo mmoja baada ya kuondoka Nigeria, anajiuliza ikiwa maisha yake ya sasa nchini Italia yalikuwa na thamani ya maumivu aliyopitia hadi kufika huko: "Sijui hata sababu ya kuja hapa."