Ardhi yao yenye utajiri wa almasi ilichukuliwa: Sasa wanataka irudishwe

- Author, Karnie Sharp
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Safari ya kilomita 800 (maili 500) kuelekea kaskazini kutoka Cape Town, Afrika Kusini – kuna makovu yaliyoachwa na uchimbaji wa madini ya almasi.
Jamii ya watu maskini wa Nama wanaoishi katikati ya uharibifu wa mazingira kaskazini-magharibi mwa Afrika Kusini - pia wanajulikana kama Namaqualand - wanajiuliza kipi kimetokea kwa utajiri ambao ardhi yao imetoa.
Mamilioni ya pesa zilizopatikana zikiendelea kujenga nchi, lakini inaonekana hakuna mengi yaliyojengwa ndani ya eneo hilo.
Wanama, wanaokaa Afrika Kusini na Namibia, wanatokana na watu wa kuhamahama - Wakhoi na Wasan – ambao ndio wakazi wa asili wa sehemu hii.
Licha ya kushinda vita vya kisheria kuhusu haki za ardhi na uchimbaji madini zaidi ya miongo miwili iliyopita huko Richtersveld, ambayo ni sehemu ya Namaqualand, wengi katika jamii hiyo wanasema bado hawajaona faida yoyote.
Akiwa amesimama katikati ya mgodi wa zamani katika mji wa pwani wa Ghuba ya Alexander, Andries Josephs, ambaye alifanya kazi hapa miongo miwili iliyopita kabla ya kufutwa kazi, anatikisa kichwa.
"Hakuna kazi, hilo ndilo tatizo. Watu wamekwama na kila kitu kimerudi nyuma. Majengo yameanguka. Ukosefu wa ajira uko juu sana," anasema.
Historia ya Wanama na almasi

Uchimbaji wa almasi umepungua katika miaka ya hivi karibuni katika sehemu hii. Takriban kilomita moja kutoka mgodi huu ulioharibika kuna eneo la makazi lenye nyumba chache, jengo la kanisa lililoharibika na hospitali yenye madirisha yaliyoharibika, inayotoa huduma za msingi tu.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mpango wa maendeleo unaelezea miundombinu "iliyochakaa" ya maji na umeme pamoja na barabara duni zinazoathiri upatikanaji wa vitu kama vile huduma ya afya.
Karne moja iliyopita, ugunduzi uliofanywa kusini mwa Mto Orange, ambao sasa ni sehemu ya mpaka wa Afrika Kusini na Namibia, ulisababisha msongamano mkubwa ambao ulibadilisha ardhi hii.
Lakini Wanama tayari walijua kuhusu vito hivyo.
"Katika familia yetu, walikuwa wakiwafundisha watoto kuhesabu kwa kutumia almasi," anasema Martinus Fredericks.
Mwaka 2012, wazee wa Nama walimteua kuwa kiongozi wao nchini Afrika Kusini. Mzee huyo mwenye umri wa miaka 60 anasema walimhimiza kupigania kurejeshwa kwa ardhi ya mababu zao.
Wanama hapo awali walikuwa wafugaji na wafanyabiashara hadi "walowezi" wa Ulaya walipokuja na kuingilia maisha yao, kulingana na Fredericks.
Eneo waliloishi lilichukuliwa katikati ya karne ya 19 na Koloni ya Cape - sehemu ya kile ambacho sasa ni Afrika Kusini - na kisha, baada ya almasi kupatikana katika miaka ya 1920, Wanama waliondolewa kwenye ardhi karibu na Mto Orange.
Hakuna kilichobadilika katika miaka yote ya mfumo wa ubaguzi wa rangi, au baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia na mwisho wa utawala wa wachache wa wazungu mwaka 1994.
Serikali mpya inayoongozwa na African National Congress ilishikilia msimamo wa awali kwamba faida kubwa zaidi ilipatikana kwa almasi hiyo kutumika kwa faida ya na nchi nzima.
Wanama hawakuwa na furaha na wasiwasi huo unaendelea hadi leo.
"Unaenda katika eneo kama Richtersveld... unaona jinsi watu walivyo maskini,"Fredericks anasema. "Hawana ajira.”
"Sipingi maendeleo, lakini lazima yawe kwa kiwango ambacho jamii inafaidika kama mshirika."
Kesi mahakamani

Baada ya miaka mitano ya kesi ya kisheria na serikali na kampuni ya madini inayomilikiwa na serikali, Alexkor, ambayo iliishia katika mahakama ya juu zaidi, majaji walifanya maamuzi mwaka 2003.
Mahakama ya Katiba ilisema Wanama wana haki katika ardhi ya mababu zao na haki ya madini yaliyopo. Hata hivyo, miaka minne baadaye, Alexkor iliingia mkataba na Richtersveld Communal Property Association (CPA), ambayo inaelezwa kuwakilisha WaNama, chama hicho kiliipa kampuni hiyo 51% ya haki katika madini huku 49% ikienda kwa jamii na chombo kinachoitwa Kampuni ya Madini ya Richtersveld.
Lakini Fredericks anasema CPA haikuwakilisha Nama na makubaliano hayo yalifanywa bila idhini ya jamii. Anadai miaka 20 baadaye bado hawajafaidika kutokana na makubaliano hayo, au kutokana na utajiri wowote uliopatikana kwa miongo kadhaa licha ya uamuzi wa Mahakama ya Katiba.
Kampuni ya Alexkor inapinga hilo, ikisema katika taarifa kwa BBC kwamba "si sahihi kusema kwamba jamii haijafaidika na ardhi yao."
Inasema Alexkor ililipa randi milioni 190 ($11m; £8.4m) "kama fidia" kwa Kampuni ya Uwekezaji ya Richtersveld (RIHC) kwa kipindi cha miaka mitatu, pamoja na randi milioni 50 ($2.9m) kama ruzuku ya maendeleo.
Ufisadi

Lakini mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Alexkor, Dineo Peta, ambaye alichukua madaraka mapema mwaka huu, anasema kampuni hiyo "ilikuwa inajua kuwa jamii haijapata faida ya kiuchumi kutokana na shughuli hizo."
Katika mahojiano na BBC alilaumu hilo kwa "utawala mbaya na utovu wa nidhamu ndani ya Alexkor."
Uongozi wa awali ulifanyiwa uchunguzi na tume maalum. Ripoti ya tume ya 2022 iligundua kuwa kumekuwa na ufisadi - matokeo hayo kwa sasa yanachunguzwa lakini hayajasababisha kupatikana hatia kwa mtu yoyote.
Pesa zilizokabidhiwa kwa CPA, ziliibuliwa katika kikao cha bunge cha hivi karibuni. Mbunge mmoja, Bino Farmer, alisema, Kamati Teule ya Kilimo, Mageuzi ya Ardhi na Rasilimali za Madini ilisikia kutoka kwa idara ya maendeleo ya vijijini kwamba CPA "haifanyi kazi vizuri."
Aliongeza kuwa "pia ilibainika kuwa zaidi ya randi milioni 300 ($17.6m) zimelipwa na idara na bado watu wa jamii hawakupokea chochote."
CPA haikuwepo katika kikao hicho lakini mwenyekiti wa kamati teule alisema, idara husika za kitaifa hazikutekeleza vya kutosha agizo la Mahakama [ya Katiba]".
BBC iliwasiliana na CPA mara kadhaa katika juhudi za kuelewa kilichotokea kwa pesa hizo lakini haijapata jibu.
"[Sisi] tungepaswa kuwa katika hali nzuri zaidi kwa sababu sisi ndio walinzi wa awali wa ardhi," Fredericks anasema.
Uharibifu wa Mazingira

Mbali na pesa, kiongozi wa jamii ana wasiwasi mwingine: mazingira.
"Makampuni makubwa huja, yanaharibu ardhi, yanachukua chochote yanachoweza, na yanaondoka tu bila kufanya ukarabati, na kuacha jumuiya na madhara ya uchimbaji wao," anadai.
"Wanama walikuwa wakichimba madini wenyewe, lakini wakifanya hivyo kwa njia nzuri, walijua jinsi ya kutumia rasilimali kutoka kwenye ardhi lakini pia jinsi ya kurekebisha ardhi baada ya kuitumia."
Uharibifu ulioachwa na uchimbaji madini wa kibiashara ni vigumu kuukosa. Baadhi ya migodi bado imeachwa, na hakuna dalili ya ukarabati. Kuna ushahidi wa uchimbaji, ambapo ardhi imechimbwa, na kuacha mandhari isiyopendeza.
Mgodi huko Hondeklipbaai, ambao hapo awali ulikuwa unamilikiwa na kampuni kubwa ya uchimbaji madini, Trans Hex, umetelekezwa.
Hii si sehemu ya eneo la Richtersveld lakini bado inachukuliwa kuwa ardhi ya Nama.
Katika barua kwa BBC, Trans Hex inasema iliuza eneo hilo miaka mitano iliyopita, lakini "ilikuwa na haki ya uchimbaji madini, ilifuata taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja na kuweka bajeti ya fedha kwa ajili ya ukarabati wa maeneo ya uchimbaji madini."
Lakini sasa kwa kuwa imeuza eneo hilo, Trans Hex haina jukumu tena la ukarabati, iliongeza.
Kampuni nyingine kubwa ya uchimbaji madini, De Beers, imeuza hisa zake katika migodi iliyoko pwani ya magharibi na inasema ilifanya ukarabati wa mazingira.
Lakini katika barua pepe kwa BBC imesema "kama sehemu ya makubaliano ya mauzo mwaka 2023 na Kleinzee Holdings, De Beers Consolidated Mines ilitoa randi milioni 50 ($3m) kusaidia kazi ya ukarabati katika eneo hilo."
Sasa kuna wasiwasi kwamba uharibifu wa mazingira unaweza kwenda kusini zaidi huku makampuni ya madini yakielekea pwani.
BBC iliiuliza Wizara ya misitu, uvuvi na mazingira kujibu madai kwamba makampuni mengi ya madini hayakarabati ardhi vya kutosha.
Dion George, aliyekuwa waziri hadi mwezi uliopita, amesema hawezi kusema chochote akiongeza kuwa kuwasiliana kupitia vyombo vya habari "hakuna msaada na hakuleti maendeleo."
Waziri mpya, Willie Aucamp, anayehudumu chini ya mwezi mmoja tu, hayuko katika nafasi ya kutoa maoni bado.
Lakini Fredericks anasema, “serikali inapaswa kurudisha kile kilicho chetu.”
Ili kubadilisha mambo, ameanza hatua za kisheria dhidi ya CPA, kundi ambalo lilipaswa kuendesha mambo kwa niaba ya jamii yake.
"Wanama hawawezi kuwa watu wa Nama bila udhibiti wa ardhi ya Nama. Mtu wa Nama hawezi kutenganishwa na ardhi ya Nama kwa sababu ya uhusiano wa ndani kati ya mtu huyo na ardhi."















